1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Ulinzi wa Ukraine kuondolewa katika wadhifa wake

Daniel Gakuba
6 Februari 2023

Mbunge mwenye ushawishi mkubwa nchini Ukraine amesema waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Oleksii Reznikov ataondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na mkuu wa ujasusi jeshini, kutokana na tuhuma za ufisadi jeshini.

https://p.dw.com/p/4N8F1
Ukraine Oleksij Resnikow
Waziri wa ulinzi wa Ukraine Oleksii Reznikov anayetarajiwa kuondolewa katika wadhifa huoPicha: Genya Savilov/AFP/Getty Images

Waziri huyo wa ulinzi wa Ukraine amekuwa akikabiliwa na shinikizo la kumtaka ajiuzulu, baada ya kuibuka tuhuma za ufisadi jeshini, lakini amekuwa akilikidi shinikizo hilo, akisema ataachia ngazi ikiwa tu atatakiwa kufanya hivyo na Rais Volodymyr Zelenskiy.

Soma zaidi: Urusi na Ukraine zabadilishana wafungwa wa kivita

Hata hivyo, mbunge mmoja mwenye nguvu nchini Ukraine, David Arakhamia amesema jana jioni kuwa Reznikov angeondolewa kutokana na kashfa hiyo ya ufisadi ambayo imemlazimisha naibu wake kujiuzulu.

Arakhamia amesema vita vinaweka ushawishi katika sera zinazohusu wafanyakazi, na kwamba mkuu wa ujasusi jeshini Kyrilo Budanov angeteuliwa kuwa waziri mpya wa ulinzi. Mbunge huyo amesema waziri Reznikov atahamishiwa katika wizara nyingine, bila hata hivyo kubainisha muda yatakapofanyika mabadiliko hayo.

Zelenskiy asema shinikizo la Urusi linazidi kuwa kubwa

Hayo yanajiri wakati rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akiarifu kuwa Urusi inaongeza kwa kiasi kikubwa mashambulizi yake mashariki mwa Ukraine, kwa kuzidisha idadi ya wanajeshi. Zelenskiy amesema harakati hizo za Urusi ni juhudi za kufidia kipigo kikali ilichokipata mwaka jana kutoka kwa Ukraine ambacho amesema kiliipa Urusi hasara kubwa kijeshi.

Ukraine Krieg Bachmut
Mji wa Bakhmut mashariki mwa Ukraine unakabiliwa na mapigano makaliPicha: Oleksandr Ratushniak/REUTERS

Kiongozi huyo amesema Urusi inatumia njia nyingi katika kampeni yake hiyo, zikiwemo mbinu za usambazaji wa taarifa, na kuongeza kuwa lazima Ukraine isimame imara.

''Hali ni mbaya sana katika mkoa wa Donetsk, lakini, bila kujali ukubwa wa changamoto na shinikizo, lazima tustahimili,'' amesema Zelenskiy na kuongeza kuwa wanapaswa kutumia muda wote kuimarisha ulinzi wao kwenye mstari wa mbele. ''Ni lazima kuwapa watu wetu fursa mpya ya kujinusuru katika wakati huu mgumu.Hatuna chaguo jingine bali kujilinda na kupata ushindi,'' amesema.

Jana mapigano makali yaliripotiwa katika mji wa Bakhmut ambao Urusi imeulenga kwa muda mrefu, na makombora kadhaa ya Urusi yalianguka katikati mwa mji wa Kharkiv ambao ni makao makuu ya mkoa wa Kharkiv wa kaskazini mashariki mwa Ukraine.

Deutschland Waffen für die Ukraine
Ujerumani imekubali kuipatia Ukraine vifaru 14 chapa Leopard 2Picha: Martin Meissner/AP Photo/picture alliance

Kansela Scholz asema silaha za Ujerumani hazitatumiwa kuilenga ardhi ya Urusi

Wakati Ukraine ikiwaomba washirika wake wa magharibi kuharakisha upelekaji wa msaada wa silaha ilioahidiwa, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema anayo makubaliano na rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kwamba vifaru na silaha nyingine ambazo Ujerumani itaipatia Ukraine havitatumiwa kufanya mashambulizi katika ardhi ya Urusi.

Soma zaidi: Ujerumani yakubali kuipatia Ukraine vifaru chapa Leopard 2

Akizungumza na gazeti la kila siku la Bild la hapa Ujerumani, Kansela Scholz kila hatua ya kuipatia silaha Ukraine inatafakariwa kwa kina, kwa ushirikiano na washirika wengine, hususan Marekani.

Baada ya wiki kadhaa za kusitasita, hatimaye Ujerumani ilikubali kuipatia Ukraine vifaru 14 vya mashambulizi chapa Leopard 2, sambamba na msaada mwingine kama huo utakaotoka Marekani na Uingereza kuelekea Ukraine.

 

Vyanzo: dh, zc/sms, fb (AFP, Reuters, dpa, AP)